Saturday, August 11, 2018

UJASIRIAMALI 2

KABLA YA KUANZISHA BIASHARA YAKO HAKIKISHA UNA SIFA ZIFUATAZO:
Nidhamu binafsi – Hakuna mjasiriamali anayependa kuona biashara yake inakufa, kila mmoja analenga kuhakikisha biashara inafanikiwa na huondosha kila jambo linaloweza kuhatarisha ustawi wa biashara husika. Wajasiriamali waliofanikiwa wana nidhamu ya kuchukua hatua kila siku kuelekea kwenye kufanikisha malengo yao. Hakikisha unanidhamu ya kutunza mda na nidhamu ya kutumia pesa zinazopatikana kutokana na biashara yako.
Kujiamini – Mjasiriamali hupaswi kuwa na wasiwasi kuwa unaweza kufanikiwa au la, unapaswa kujiamini mda wote kuwa utafanikisha biashara yako. Jitahidi kudhihirisha kujiamini huko kwa kufanya kazi kwa bidii ili kifikia malengo uliyojiwekea.

Muwazi wa fikra – Mjasiriamali anatambua kuwa kila tukio au hali ni fursa ya kibiashara. Mawazo mapya yanaibuliwa kila mara kuhusu mtiririko wa kazi na ufanisi, ujuzi, na biashara mpya. Mjasiriamali ana uwezo wa kutizama kila jambo [hali/ tukio] linalomzunguka na kulitumia kufanikisha lengo lake.

Muanzilishi  Mjasiriamali anafahamu kuwa kama kuna jambo linalopaswa kufanyika basi yeye mwenyewe ndiye anayepaswa kulianzisha. Hujiwekea vigezo na kuhakikisha biashara inafuata kuelekea kutekeleza/ kukidhi vigezo hivyo. Wako makini katika kutwaa fursa bila kuhitaji kusubiri mtu mwingine awape fursa

Mshindani – Chanzo cha biashara nyingi ni mjasiriamali mmoja kutambua kuwa anaweza kufanya biashara hiyo kwa ubora kuliko mwingine/ wengine. Wajasiriamali wanahitaji kufanikiwa katika biashara wanazoanzisha mithili ya mchezaji anavyohitaji kushinda katika mchezo anaocheza. Mjasiriamali ni mwepesi kuonesha namna taasisi yake ilivyofanikiwa katika hatua mbalimbali.

Mbunifu – mojawapo ya mambo muhimu katika ubunifu ni kumudu kuunganisha mambo ambayo hayaonekani kuwa na uhusiano katika kutengeneza fursa. Wajasiriamali huja na suluhisho baada ya kuchambua na kutengeneza uhusiano wa hali/ matukio mbalimbali. Huweza hata kubadili malengo ya bidhaa fulani na kuiuza katika soko tofauti.

Kutokata tamaa – Wajasiriamali hawakatishwi tamaa na kushindwa. Kila anaposhidwa huichukulia kama fursa ya kujifunza na kufanikiwa. Wanatamani kila wanalofanya lifanikiwe, hivyo hujaribu tena na tena hadi wafanikiwe. Hawaamini kuwa kuna jambo lisilowezekana

Ujuzi binafsi – Mjasiriamali ana ujuzi mzuri wa kuwasiliana katika kuuza na kuwapa motisha waajiriwa wao. Wajasiriamali wengi waliofanikiwa hufahamu namna ya kuwapa motisha waajiriwa wao hivyo kukuza biashara zao. Ni wazuri katika kuelezea faida za hali mbalimbali na kuwafundisha wengine katika kufanikiwa.

Mwenye kuheshimu maadili ya kazi yake – Mjasiriamali hufanikiwa kwa kufuata/ kutii kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika. Mifano ya wajasiriamali wasio na maadili ni: Muuzaji wa matunda anayeokota matunda kutoka kwenye shimo la taka kwa ajili ya kuwatengenezea wateja wake sharubati (juisi), au mjasiriamali anayeuza nyama isiyokaguliwa au iliyokatazwa kwa matumizi ya binadamu.

Mwenye kupenda kazi yake – Kupenda na kuthamini kazi yake ni sifa muhimu kuliko zote anayohitaji mjasiriamali ili kufanikiwa. Mjasiriamali ana mapenzi ya dhati kwa kazi yake. Yuko tayari kufanya kazi saa za ziada kuhakikisha biashara yake inafanikiwa, maana hupata furaha kuona biashara inafanikiwa. Mjasiriamali anayefanikiwa ni yule ambaye hujifunza bila kuchoka na kutafiti namna mbalimbali za kufanya biashara yake iwe bora zaidi.

Wajasiriamali wanaofanikiwa hutizama biashara zao kama mtu aliye juu ya kilima na kuona biashara yake ilivyo. Akishaiona, anataka kwenda mbali zaidi. Wanafahamu namna ya kuzungumza na waajiriwa wao, na biashara zao hutanuka kwa sababu hiyo.

No comments:

Post a Comment